Monday, May 9, 2016

KALENDA YA UFUGAJI NYUKI TANZANIA.

KALENDA YA UFUGAJI NYUKI TANZANIA.


Kalenda ya Ufugaji Nyuki ni mwongozo kwa Mfugaji Nyuki kujua majira katika eneo analofugia ili kuweza kupanga ratiba ya kazi za kusimamia makundi ya Nyuki.Katika nchi za kitropiki kuna vipindi vya kiangazi na vipindi vya mvua sio kama nchi za baridi ambapo kuna majira ya vipindi vinne kwa mwaka.Kalenda ya Ufugaji Nyuki Tanzania imegawanyika katika misimu minne kulingana na majira kwa mwaka ambayo hutofautiana kati ya mkoa na mkoa.
Katika kila msimu kazi za mfugaji Nyuki hutegemea kundi la Nyuki linahitaji nini na mfugaji afanye nini kuweza kuzalisha mazao ya Nyuki.

MSIMU WA NJAA KWA NYUKI
Ni kipindi cha kiangazi ,ukame na mimea mbalimbali imepukutisha maua na majani.
Matokeo.
·        Chakula kinakuwa kidogo kwenye mzinga
·        Idadi ya Nyuki hupungua mzingani
·        Malkia hupunguza au huacha kutaga mayai kabisa.
·        Makundi ya Nyuki kuhama kutafuta sehemu zenye malisho(ubichi)
·        Baadhi ya makundi ya Nyuki hupita kwenye kundi lenye asali kuiba.
Wajibu wa Mfugaji Nyuki katika msimu huu.
·        Chukua tahadhari ya mizinga usivamiwe na maadui wa nyuki mfano sisimizi,nyegere na wengine wanaotaka kuingia ndani ya mzinga.
·        Makundi yakingwe kutokana na jua kali na upepo.
·        Andaa vifaa vya ufugaji nyuki(kutengeneza mizinga,kukarabati iliyo mibovu)
·        Lisha makundi ya Nyuki imara kwa asali kama njaa ni kali.
MSIMU WA KUJIJENGA KWA NYUKI.
Hiki ni kipindi ambapo mvua za awali zimeanza na mimea inachanua kwa wingi.Makundi ya Nyuki hupita kutafuta makazi pia huzungukazunguka kwenye mzinga na sehemu nyingine.
Matokeo
·        Nyuki hujenga masega ya asali
·        Nyuki huzaliana kuongeza idadi yao kwenye mzinga
·        Makundi ya Nyuki hupita kutafuta makazi
·        Makundi huhama kwenye mizinga endapo kuna maadui au mzinga kuwa mbovu.
Wajibu wa Mfugaji Nyuki katika Msimu huu.
·        Fanya ukaguzi wa mizinga na manzuki kuwa katika hali ya usafi.
·        Safisha na kuambika mizinga isiyo na  Nyuki.
Tafuta makundi ya Nyuki ili kuwezesha mizinga kuwa na Nyuki kwa njia ya;
Ø Kutundika mizinga ya kukamatia makundi sehemu ambapo makundi ya Nyuki hupitapita.
Ø Kugawa makundi makubwa.
Ø Kuzalisha makundi ya Nyuki.
·        Saidia Nyuki kuongeza kiota kwa kuweka sanduku la ziada
·        Hakikisha Nyuki wana chakula cha kutosha
·        Kagua mizinga ya kisasa ya viunzi na vuna mzinga uliobebeshwa endapo una asali iliyokomaa
·        Tembelea mara kwa mara mizinga yenye makundi ya Nyuki kuona maendeleo au matatizo.
MSIMU WA MTIRIRIKO WA ASALI KWA NYUKI.
Ni kipindi ambapo miti na vichaka vimechanua maua kwa wingi na Nyuki wanatembelea maua kukusanya mbochi na chavua.Wakati huu ukipita karibu na mimea yenye maua utasikia sauti za Nyuki.
Matokeo.
·        Nyuki hukusanya mbochi na kuibadilisha kuwa asali.
·        Maadui wa Nyuki mfano siafu,sisimizi na wengineo huongezeka jirani na kundi la Nyuki.
·        Nyuki huongezeka kwenye kundi pamoja na kutengeneza masega.
·        Nyuki hupita kutafuta maji.
·        Weka kumbukumbu za maendeleo ya kila kundi na manzuki
·        Jenga ushirikiano na wafugaji Nyuki jirani kwa ajili ya kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwa pamoja.
Wajibu wa Mfugaji Nyuki katika msimu huu.
Ø Fanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye manzuki na mizinga ya Nyuki.
Ø Fyeka majani na matawi ambayo yanasonga mizinga ya Nyuki.
Ø Wekea vizuia wadudu kupanda  kwenye mzinga wa Nyuki wa Nyuki hasa ile inayokaa kwenye vichanja
Ø Weka masanduku ya ziada kubebesha kwenye mizinga ya viunzi ili kuongeza uzalishaji,
Ø Fanya maandalizi ya vifaa vya kuvunia na kuhifadhia asali.
Ø Vuna baadhi ya masanduku yaliyobebeshwa endapo yana asali.
Ø Anza kutafuta masoko ya Asali unayokadiria kuvuna.
Ø Weka kumbukumbu za maendeleo ya kila kundi.
MSIMU WA MAVUNO KWA MFUGAJI NYUKI.
Ni kipindi ambapo maua ya mimea yamepungua na kuanza kutoa mbegu ama matunda,kiangazi ndio kinaanza.Sehemu nyingine baada ya kuisha mvua za vuli.Ni matunda ya kazi ya misimu mitatu iliyotajwa hapo juu na ni jukumu la Mfugaji wa Nyuki kuvuna mazao ambayo nyuki wamemuandalia.
Matokeo.
·        Nyuki huongeza ulinzi nje ya mzinga na huwa wakali
·        Baadhi ya mizinga nyuki hujikusanya nje.
·        Nyuki hupunguza kupitapita kwenye maua au kuhama.
Wajibu wa Mfugaji Nyuki katika Msimu huu.
·        Vuna masega yenye asali iliyokamaa.
·        Tumia bomba la moshi,mavazi ya kinga na vyombo safi wakati wa kuvuna.
·        Bakiza masega kiasi yenye asali kuwezesha Nyuki kutumia kama akiba.
·        Chuja asali na kuhifadhi katika eneo sahihi kulingana na ushauri wa kitaalamu.
·        Andaa nta endapo masega yametoka kwenye mizinga ya miche.
·        Tafuta masoko na kuuza mazao ya Nyuki.
·        Weka kumbukumbu za mavuno kwa kila mzinga na manzuki.
·        Toa taarifa zinazohusiana na mavuno na mauzo ya mazao ya Nyuki kwa Maafisa Ugani waliokaribu.

MABADILIKO YA KALENDA YA UFUGAJI NYUKI.
Sehemu ambazo zinapata mvua za vuli na masika kuna kuwa na msimu mdogo wa mavuno na msimu mkubwa wa mavuno.
Msimu mdogo wa mavuno huwa ni katika kipindi cha;
Mwezi Disemba/Januari(siku 14 tu) – Misitu ya miombo.
Mwezi February(Siku 14 tu) – Vichaka vya nang’ana.
ANGALIZO: EPUKA KUCHEMSHA ASALI.Asali iliyokamuliwa vyema na kuhifadhiwa vizuri mahali pasafi bila kuchemshwa huwa ASALI MBICHI ILIYO BORA.

Kwa maoni/Ushauri niandikie;
fabianbalele@gmail.com