Tuesday, September 30, 2014

MASWALI YANAYOULIZWA MARA KWA MARA KUHUSU UFUGAJI WA NYUKI





UFUGAJI WA NYUKI NI NINI?
Ufugaji wa Nyuki ni kuhifadhi nyuki ndani ya Mizinga kwa Madhumuni ya  kupata mazao ya nyuki kama vile asali,nta na gundi

NYUKI HUFUGWA WAPI?
Nyuki wanaweza kufugwa mahali popote penye mimea inayotoa maua ya kufaa.
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA UNAPOCHAGUA SEHEMU YA KUFUGIA NYUKI.
1)Chunguza kama ipo Mimea ya Maua ya kufaa na kutosha,kwa mfano uoto wa asili kama vile miombo,au mashamba ya miti au mazao ya kilimo.
2) Chunguza Kama kuna maji ya kutosha naya kudumu.Endapo hakuna maji hakikisha unaweka maji kwa kuwajengea visima vidogo vidogo au hata kwenye madebe au makopo.
3) Chunguza kama pana athari za mafuriko ya mara kwa mara ili mizinga yako usizolewe na maji.
4) Chunguza kama sehemu uliyochagua inapitika nyakati zote za mwaka na ina kivuli cha kutosha 
5) Chunguza kama sehemu uliyochagua haina upepo mkali kupita kiasi. Upepo mkali unaozidi kilometa 80 kwa saa utazuia nyuki kutoka nje au kupotea kwa kusombwa na upepo.
6) Chunguza kama sehemu hiyo haina maadui wa mizinga  na nyuki kwa mfano nondo, nyegere, wezi, mchwa, siafu n.k.
7) Hakikishha sehemu utakayochagua iko mbali na barabra kuu au shughuli za jumuiya, mfano, soko, kanisa, msikiti, shule, makazi ya watu, hospitali n.k.
IDADI GANI YA MIZINGA IWEKWE KWENYE MANZUKI?
Idadi ya mizinga inayotakiwa kuwekwa kwenye manzuki inategememea wingi na aina ya mimea inayotoa maua katika  sehemu husika. Inashauriwa kutokuweka mizingi mingi kupita uwezo wa eneo la kufugia nyuki.
Makadirio ya idadi ya mizinga kwenye eneo la mita 120 za mraba katika uoto mbalimbali yameoneshwa kwenye jedwali namba 1
Jedwali Na 1: Idadi ya mizinga kwenye eneo la mita za mraba 120 kwa maeneo mbalimbali
NA
AINA ZA UOTO
IDADI YA MIZINGA
1
Miombo yenye miti mingi
5 - 10
2
Miombo yenye miti ya hapa na pale
5
3
Misitu minene
15 au zaidi
4
Misitu ya kupandwa yenye miti inayotoa maua
15 au zaidi
5
Shamba la katani
15 au zaidi
6
Shamba la Michungwa
15 au zaidi
7
Shamba la mazao ya kilimo mchanganyiko
5
8
Mkusanyiko wa uoto anuai kama vile vichaka na mbuga za majani.
2 - 4

JINSI YA KUTEGA MAKUNDI YA NYUKI ILI KUANZINSHA MANZUKI
1.    Mizinga mipya kabla ya kutundikwa ni budi iwekwe chambo. Chambo kinachotumika zaidi ni nta. Nta iliyoyeyushwa na kupakazwa ndani ya mzinga hutoa harufu ambayo huwavutia nyuki. Mizinga iliyowekwa chambo hutundikwa juu ya miti kwa kutumia waya kusubiri makundi ya nyuki yapite.
2.   Njia nyingine ni kugawa kundi kubwa la nyuki na kugawia kwenye mzinga mpya au usiokuwa na nyuki. Masenga mawili, moja lenye majana na mayai na moja lenye asali au chavua pamoja na nyuki wasiopungua 100 huhamishwa kwenye mzinga mpya. Mzinga uliogawiwa nyuki (mpya) unawekwa pale ambapo mzinga wa zamani ulipokuwa na wa zamani unahamishwa.
3.   Njia nyingine ni kukamata makundi ya nyuki yaliyojikusanya kwenye tawi la mti na kulikung’utia ndani ya boksi au mzinga mdogo halafu unakwenda kuwaweka kwenye mzinga wako mpya. Nyuki hawa itabidi walishwe siku za mwanzo kwa kutumia asali au shira ya sukari kwa vile  watakuwa hawana chakula.
MAMBO YA KUFANYA KWENYE SHAMBA LA NYUKI
Utunzaji ya nyuki /shamba la nyuki kunalenga kupata mazao bora na ya kutosha ya asali na nta, pia faida zitokanazo na uchavushaji wa nyuki kwa mazao mbalimbali ya kilimo.
Katika kuhudumia makundi yako ya nyuki unahitajika kuwa na kalenda ya mfuga Nyuki. Kalenda ya mfuga nyuki ni utaratibu wa shughuli zote mfugaji anazotakiwa kuzifanya katika kipindi cha mwaka. 
Kalenda ya mfugaji nyuki inatambulika mfugaji shughuli gani ya kufanya na ambayo haijafahamika katika misimu mbalimbali ya mwaka.
Aidha,  ukaguzi wa makundi na uvunaji wa asali hufanywa kulingana na kalenda  ya ufugaji nyuki.
Kalenda za ufugaji wa nyuki hazifanani kwa kila eneo  la nchi. Hii inatokana na majira ya mwaka ambayo nayo ni tofauti tofauti kufuatana na sehemu ya nchi.
Yafuatayo ni maelezo ya kalenda ya mfuga nyuki pamoja na shughuli zinazohitaka kufanywa;
     Msimu wa njaa
Hiki ni kipindi cha kiangazi ambacho maua kwa ajili ya mbochi na chavua yameadimika . Aidha, akiba ya asali na chavua kwa ajili ya nyuki ni kidogo.
  
      Shughuli za kufanya katika kipindi hiki ni zifuatazo
·        Kukagua makundi kuangalia maadui wa nyuki, mfano, siafu, nondo n.k.
·        Kuwalisha nyuki, kwa kutumia shira ya sukari , au asali kama ipo ikiwa nyuki hawana akiba yeyote iliyosalia. Angalizo:Hapa Tanzania hakuna mazoea ya kulisha nyuki  isipikua mkulima/mfugaji akiamua mwenyewe.

Jinsi kulisha nyuki
·        Tengeneza mchanganyiko wa sukari na maji . sehemu 1 kwa 1 yaani kikombe 1 sukari na maji kikombe 1.
·        Chemsha maji mpakaka yachemke kisha ondoa motoni na ongeza sukari huku ukikoroga mpaka iyeyuke. 
·        Acha mchanganyiko upoe
·        Jaza mchanganyiko kwenye chombo cha kulishia nyuki
·        Angalia baada ya  siku tatu ili ikibidi uwaongezee nyuki chakula

Msimu wa kujenga
Huu ni msimu wa nyuki wa kujenga, kwani kipindi hiki vichaka pamoja na miti michache inaanza kutoa maua na nyuki wanaanza kujenga masega ya kuweka asali tayari kwa msimu ujao  wa maua. Aidha , Malkia anataga mayai zaidi na nyuki wengi zaidi hutotolewa ili kuongeza nguvukazi kwente kundi la vubarua  kwani wengi watakuwa wamekufa kipindi cha njaa.
Shughuli za kufanya katika kipindi hiki ni zifuatazo
·        Kagua maadui wa nyuki katika mizinga
·        Unganisha makundi madogo ili kupata kundi kubwa
·        Kugawa baadhi ya makundi ikiwa ni makubwa ili yahamishiwe kwenye mizinga iliyohamwa. 
·        chunguza kama nyuki wanajenga masega vizuri kwehye vinzi au miche na siyo kwa kukatiza
·        usafi wa shamba

Msimu wa maua
Wakati huu vichaka vingi na mimea mingi inatoa maua,  nyuki wanakusanya chakula(mbochi na chavua ) kwa wingi pamoja na kuivisha asali.
Shughuli za kufanya katika kipindi hiki ni zifuatazo:
·        kupanua viota (kwa mizinga ya biashara), ina maana kuwa kama sanduku la chini limekaribia kujaa yaani liko robo tatu basi uongeze jingine la ziada juu yake baada ya kuweka kitenga malkia.
·        Kuangalia maadui.
·        Kuangalia kama asali imeshaiva na tayari kwa kuvuna
·        Kutafuta soko la kuuzia mazao yako(Asali,Nta,Gundi n.k)

Makala hii itaendelea tena………….
Imeandaliwa kwa Msaada wa kitabu cha  (R.P.C Temu,2007 ). Na msaada wa Mtandao/Internet.

Kwa Maoni /Ushauri: +255714759047/+255768937884

                        fabianbalele@gmail.com

No comments:

Post a Comment