Monday, December 28, 2015

Mambo 10 Usiyoyajua Kuhusu Maisha ya "Nyuki"


1)Nyuki Malkia ni mkubwa kuliko Nyuki wengine katika kundi la Nyuki.
2)Nyuki Malkia ni jike pekee katika kundi la Nyuki mwenye uwezo wa kimaumbile wa kutaga mayai ingawaje kwenye kundi la Nyuki kuna majike wengi.
3)Nyuki Malkia ndiye Nyuki pekee mwenye uwezo wa kuishi muda mrefu zaidi,miaka mitatu hadi sita.
4)Nyuki VIBARUA ni majike ambao maumbile yao hayana uwezo wa kutaga mayai wala kujamiiana.
5)Nyuki dume hutokana na mayai ya Malkia yasiyorutubishwa na mbegu za kiume na kuwafanya nyuki hao kuwa na mzazi mmoja pekee yaani mama.
6)Nyuki dume hawana mshale wa sumu kwa ajili ya kujilinda dhidi ya maadui,badala yake wana uume.
7)Dume mmoja huweza kujaniiana na Malkia Mara moja tu ktk maisha take.
8)Baada ya tendo la kujamiiana Nyuki Dume hufa SAA chache kutokana na uume wake kukatika wakati wa kujamiiana.
9)Kwa hali hii,hata Nyuki vibarua hawajawahi kuwaona baba zao.
10)Kuna takribani aina tofauti elfu ishirini (20,000) za Nyuki wanaouma Duniani.



©Exclusive to "Balele Mwanahabari"..


Kwa maoni/Ushauri
0768937884 
fabianbalele@gmail.com

SIFA ZA SHAMBA LA NYUKI (MANZUKI)


Kuwapo Kwa mimea inayotoa Maua yanayotoa chakula cha nyuki cha kutosha, Kwa mfano,sehemu yenye misitu, shamba la miti au mazao ya kilimo. Muda wa mimea kuchanua ujulikane kwa mfugaji nyuki ili aweze kupanga muda ambao atawezesha kundi la nyuki kujijenga na kukusanya mazao ya kutosha wakati mimea inapochanua Maua. 

Maji ya kutosha ni muhimu, nyuki huyatumia kupooza kupooza joto ndani ya mzinga, kulainisha chakula na kurekebisha utamu wa asali ambayo hulishwa majana. 

Mahali panapofikia ili kuwezesha usafirishaji wa vifaa na mazao ya nyuki nyakati za uvunaji. 

Umbali wa kilomita tatu kutoka katika makazi ya watu,shule,hospitali na pasiwe mahali ambapo ni mapito ya Mifugo. Inapolazimu kuwa na Manzuki katika maeneo haya ,izungushiwe uzio wenye miti mirefu ili nyuki wanapokwenda nakurudi kutafuta cha kula wapiti juu  ili wasishambulie watu na wanyama. Umbali uliotajwa hapa ni kwa ajili ya nyuki  wanaouma tu. 

Mbali na maeneo ya kilimo kinachotumia kemikali kwa mfano kilimo cha tumbaku na korosho, Manzuki yaanzishwe umbali wa kilometa saba kutoka maeneo hayo. Hii ni kuzuia nyuki wasife kwa kemikali hizo, au kuzuia mizinga isiangushwe na pia kusababisha nyuki washindwe kurudi kwenye mizinga.
Kudhibiti uharibifu kutokana na maadui wa nyuki, wizi wa mizinga na mazao ya nyuki.

Viashiria Vifuatavyo hutumika sehemu mbalimbali kutambua muda wa kuvuna Asali..
i)Mwisho wa Msimu wa mvua na mwanzo wa Kangazi

ii)Maua au matunda ya mmea Fulani kupukutika

iii)Matunda ya mmea mwitu kutokeza

iv) Mazao ya shamabani kukomaa

v)Mng’urumo wa nyuki wakusanyao chakula kupungua

vi)Madume ya nyuki kuonekana yamekufa kwenye mlango ama chini ya mzinga

vii)Kundi la Nyuki kutanda nje ya Mzinga

viii)Gundi nyingi kuonekana katika mlango na matundu ya Mzinga

ix) Uzito wa Mzinga kuongezeka

x)Kijiti kuchomwa ndani ya Mzinga na kuona kama kina asali(Ukaguzi wa kienyeji)Njia hii haimuwezeshi mfugaji kujua kama asali imeiva ama mbichi.

xi)Sauti ya mzinga unapogongwa,inaashiria kama mzinga umejaa ama ni mtupu.

xii)Mwinamo wa mzinga kubadilika.
Muda wa Uvunaji asali baada ya kundi kuingia kwenye mzinga hutegemea mambo yafuatayo;
i)Kiwango cha maua yanayopatikana kwenye eneo la shamba la nyuki.

ii)Muda ambao maua hayo yanapatikana.

iii)Hali ya Hewa ya eneo hilo

iv)Ukubwa wa Kundi

v)Uwezo wa Nyuki kukusanya Nekta



KWA MAONI/USHAURI  
0768937884
fabianbalele@gmail.com




 

AINA ZA NYUKI NA TABIA ZAO


Nyuki ni jamii ya wadudu wenye jozi mbili za mabawa mepesi yenye mishipa laini.Nyuki huishi maisha ya kijamaa.Mwili wa Nyuki umegawanyika katika sehemu kuu tatu;kichwa ,kifua na tumbo(fumbati).Tofauti na wadudu wengine,nyuki hutengeneza na kuhifadhi Asali kwenye masega.

Kuna takribani aina tofauti elfu ishirini(20,000) Duniani.Nyuki hawa wanatofautiana kwa maumbile,ukubwa na tabia,lakini wote wanashahabiana kwa tabia moja ya kutembelea maua ili kukusanya mbochi(maji matamu yanayotengeneza asali) na chavua(unga unaopatikana kwenye maua) kwa ajili ya chakula chao.

Kuna jamii kuu mbili za Nyuki wanaopatikana Tanzania;Nyuki wanaouma na wasiouma.

NYUKI WANAOUMA
Nyuki wanaouma wanaopatikana Tanzania wamegawanyika katika makundi matatu kutegemea mahali wanapoishi.Wapo nyuki wanaoishi;
Sehemu za Mwambao(Pwani) wana umbo dogo na niwakali(Apis mellifera litorea),sehemu kame na tambarare,wana umbo la wastani,wakali kiasi na hutoa asali kwa wingi(Apis mellifera scutellata),sehemu za milimani,(zaidi ya futi 6,000 kutoka usawa wa Bahari) wana umbo kubwa na wapole,jina la kitaalamu wanaitwa Apis mellifera monticola.

NYUKI WASIOUMA
Nyuki wasiouma wanapatikana nchi za tropiki tu kama ilivyo Tanzania.
Nyuki wasiouma wanaishi ndani ya matundu ya miti,chini ya matawi makubwa ya miti,kwenye vichuguu vya mchwa na hata chini ya mapaa ya nyumba,nyuki hawa hu toa asali kidogo kulinganisha na nyuki wanaouma,Nyuki wasiouma wanaweza kutoa hadi lita 5 za asali kwa mwaka kutegemea na ukubwa wa mzinga,aina ,wingi wa nyuki na uwepo wa chakula(maua) cha kutosha.Asali ya Nyuki wasiouma inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kutibu maradhi mablimbali kuliko asali ya Nyuki wanaouma.


JINSIA YA NYUKI NA MAJUKUMU YAO.
Kama ilivyo kwa viumbe vyote,nyuki nao waa jinsia mbili,nyuki dume na Nyuki Jike.Jinsia hizo ndiyo msingi wa mgawanyo wa majukumu ya kazi katika kundi la Nyuki.
Kundi la Nyuki wanaouma,lina aina tatu za Nyuki ambao ni Nyuki vibarua,malkia na dume.

NYUKI JIKE.
Jinsia hii inamakundi mawili ya nyuki amabyo hutekeleza majukumu mawili tofauti.

 a)Nyuki Malkia
NYUKI MALKIA(QUEEN)
Ni nyuki jike ambaye hulelewa kwa kula chakula rasmi(maziwa ya Nyuki) na kupata matunzo maalumu kwa maisha yake yote(tangu hatua ya yai hadi uzee wake wote)Chakula hiki humwezesha kuishi kati ya miaka miwili hadi sita.
Nyuki malkia ni mkubwa kuliko nyuki wengine katika kundi la Nyuki,tumbo lake ni refu lenye rangi ya njano na dhahabu ghafi.
Nyuki Malikia,hutoa kemikali(Pheremones)mwilini mwake kutoa miongozo  kwa kundi la Nyuki.Mpangilioo wote na Mgawanyo wa kazi katika kundi la nyuki hutegemea maelekezo yake.Kundi la Nyuki lisilo na Malkia hukosa mwelekeo na huishi kwa kipindi kifupi.

b)Nyuki Vibarua
Nyuki vibarua ni majike ambao maumbile yao hayana uwezo wa kutaga mayai wala kujamiiana na nyuki madume.Kwa kawaida nyuki vibarua ambao hawatagi mayai,ni majike tasaambao hawana uwezo wa wa kutaga mayai.Aidha,hufikia kuishi hadi siku 36.Wanaweza kufikia idadi ya 60,000 au zaidi katika kundi moja.

c)Nyuki dume
Hutokana na mayai ya Malikia yasiyorutubishwa na mbegu za kiumena kuwafanya nyuki hao kuwa na mzazi mmoja tu yaani mama,Nyuki dume ni wakubwa kuliko vibarua lakini wadogo kuliko Malkia.Macho yao ni makubwa na miili yao ina rangi nyeusi,nyuki dume hawana mshale wa sumu kwa ajili ya kujilinda dhidi ya maadui,badala yake wana uume.
Kazi kubwa ya Nyuki dume ni kujamiiana na malkia.Dume mmoja huweza kujamiiana na malikia mara moja katika maisha yake.,Baada ya Tendo la kujamiiana Dume hufa saa chache kutokan na uume wake kukatika wakati wa kujamiiana.

Kwa hali hii hata Nyuki vibarua hawajawai kuwaona baba zao.!

Kazi ya pili ya Nyuki madume ni kurekebisha hali ya hewa ndani ya mzinga kwa kupasha joto kiota hasa wakati wa Usiku kwa kukumbatia juu ya kiota,sehemu ya watoto.Wakati wa upungufu mkubwa wa chakula au kiangazi nyuki madume hutolewa na vibarua nje ya mizinga na baadea hufa kwa njaa au baridi.

Kwa Maoni/Ushauri
0768937884
fabianbalele@gmail.com







Tuesday, September 30, 2014

MASWALI YANAYOULIZWA MARA KWA MARA KUHUSU UFUGAJI WA NYUKI





UFUGAJI WA NYUKI NI NINI?
Ufugaji wa Nyuki ni kuhifadhi nyuki ndani ya Mizinga kwa Madhumuni ya  kupata mazao ya nyuki kama vile asali,nta na gundi

NYUKI HUFUGWA WAPI?
Nyuki wanaweza kufugwa mahali popote penye mimea inayotoa maua ya kufaa.
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA UNAPOCHAGUA SEHEMU YA KUFUGIA NYUKI.
1)Chunguza kama ipo Mimea ya Maua ya kufaa na kutosha,kwa mfano uoto wa asili kama vile miombo,au mashamba ya miti au mazao ya kilimo.
2) Chunguza Kama kuna maji ya kutosha naya kudumu.Endapo hakuna maji hakikisha unaweka maji kwa kuwajengea visima vidogo vidogo au hata kwenye madebe au makopo.
3) Chunguza kama pana athari za mafuriko ya mara kwa mara ili mizinga yako usizolewe na maji.
4) Chunguza kama sehemu uliyochagua inapitika nyakati zote za mwaka na ina kivuli cha kutosha 
5) Chunguza kama sehemu uliyochagua haina upepo mkali kupita kiasi. Upepo mkali unaozidi kilometa 80 kwa saa utazuia nyuki kutoka nje au kupotea kwa kusombwa na upepo.
6) Chunguza kama sehemu hiyo haina maadui wa mizinga  na nyuki kwa mfano nondo, nyegere, wezi, mchwa, siafu n.k.
7) Hakikishha sehemu utakayochagua iko mbali na barabra kuu au shughuli za jumuiya, mfano, soko, kanisa, msikiti, shule, makazi ya watu, hospitali n.k.
IDADI GANI YA MIZINGA IWEKWE KWENYE MANZUKI?
Idadi ya mizinga inayotakiwa kuwekwa kwenye manzuki inategememea wingi na aina ya mimea inayotoa maua katika  sehemu husika. Inashauriwa kutokuweka mizingi mingi kupita uwezo wa eneo la kufugia nyuki.
Makadirio ya idadi ya mizinga kwenye eneo la mita 120 za mraba katika uoto mbalimbali yameoneshwa kwenye jedwali namba 1
Jedwali Na 1: Idadi ya mizinga kwenye eneo la mita za mraba 120 kwa maeneo mbalimbali
NA
AINA ZA UOTO
IDADI YA MIZINGA
1
Miombo yenye miti mingi
5 - 10
2
Miombo yenye miti ya hapa na pale
5
3
Misitu minene
15 au zaidi
4
Misitu ya kupandwa yenye miti inayotoa maua
15 au zaidi
5
Shamba la katani
15 au zaidi
6
Shamba la Michungwa
15 au zaidi
7
Shamba la mazao ya kilimo mchanganyiko
5
8
Mkusanyiko wa uoto anuai kama vile vichaka na mbuga za majani.
2 - 4

JINSI YA KUTEGA MAKUNDI YA NYUKI ILI KUANZINSHA MANZUKI
1.    Mizinga mipya kabla ya kutundikwa ni budi iwekwe chambo. Chambo kinachotumika zaidi ni nta. Nta iliyoyeyushwa na kupakazwa ndani ya mzinga hutoa harufu ambayo huwavutia nyuki. Mizinga iliyowekwa chambo hutundikwa juu ya miti kwa kutumia waya kusubiri makundi ya nyuki yapite.
2.   Njia nyingine ni kugawa kundi kubwa la nyuki na kugawia kwenye mzinga mpya au usiokuwa na nyuki. Masenga mawili, moja lenye majana na mayai na moja lenye asali au chavua pamoja na nyuki wasiopungua 100 huhamishwa kwenye mzinga mpya. Mzinga uliogawiwa nyuki (mpya) unawekwa pale ambapo mzinga wa zamani ulipokuwa na wa zamani unahamishwa.
3.   Njia nyingine ni kukamata makundi ya nyuki yaliyojikusanya kwenye tawi la mti na kulikung’utia ndani ya boksi au mzinga mdogo halafu unakwenda kuwaweka kwenye mzinga wako mpya. Nyuki hawa itabidi walishwe siku za mwanzo kwa kutumia asali au shira ya sukari kwa vile  watakuwa hawana chakula.
MAMBO YA KUFANYA KWENYE SHAMBA LA NYUKI
Utunzaji ya nyuki /shamba la nyuki kunalenga kupata mazao bora na ya kutosha ya asali na nta, pia faida zitokanazo na uchavushaji wa nyuki kwa mazao mbalimbali ya kilimo.
Katika kuhudumia makundi yako ya nyuki unahitajika kuwa na kalenda ya mfuga Nyuki. Kalenda ya mfuga nyuki ni utaratibu wa shughuli zote mfugaji anazotakiwa kuzifanya katika kipindi cha mwaka. 
Kalenda ya mfugaji nyuki inatambulika mfugaji shughuli gani ya kufanya na ambayo haijafahamika katika misimu mbalimbali ya mwaka.
Aidha,  ukaguzi wa makundi na uvunaji wa asali hufanywa kulingana na kalenda  ya ufugaji nyuki.
Kalenda za ufugaji wa nyuki hazifanani kwa kila eneo  la nchi. Hii inatokana na majira ya mwaka ambayo nayo ni tofauti tofauti kufuatana na sehemu ya nchi.
Yafuatayo ni maelezo ya kalenda ya mfuga nyuki pamoja na shughuli zinazohitaka kufanywa;
     Msimu wa njaa
Hiki ni kipindi cha kiangazi ambacho maua kwa ajili ya mbochi na chavua yameadimika . Aidha, akiba ya asali na chavua kwa ajili ya nyuki ni kidogo.
  
      Shughuli za kufanya katika kipindi hiki ni zifuatazo
·        Kukagua makundi kuangalia maadui wa nyuki, mfano, siafu, nondo n.k.
·        Kuwalisha nyuki, kwa kutumia shira ya sukari , au asali kama ipo ikiwa nyuki hawana akiba yeyote iliyosalia. Angalizo:Hapa Tanzania hakuna mazoea ya kulisha nyuki  isipikua mkulima/mfugaji akiamua mwenyewe.

Jinsi kulisha nyuki
·        Tengeneza mchanganyiko wa sukari na maji . sehemu 1 kwa 1 yaani kikombe 1 sukari na maji kikombe 1.
·        Chemsha maji mpakaka yachemke kisha ondoa motoni na ongeza sukari huku ukikoroga mpaka iyeyuke. 
·        Acha mchanganyiko upoe
·        Jaza mchanganyiko kwenye chombo cha kulishia nyuki
·        Angalia baada ya  siku tatu ili ikibidi uwaongezee nyuki chakula

Msimu wa kujenga
Huu ni msimu wa nyuki wa kujenga, kwani kipindi hiki vichaka pamoja na miti michache inaanza kutoa maua na nyuki wanaanza kujenga masega ya kuweka asali tayari kwa msimu ujao  wa maua. Aidha , Malkia anataga mayai zaidi na nyuki wengi zaidi hutotolewa ili kuongeza nguvukazi kwente kundi la vubarua  kwani wengi watakuwa wamekufa kipindi cha njaa.
Shughuli za kufanya katika kipindi hiki ni zifuatazo
·        Kagua maadui wa nyuki katika mizinga
·        Unganisha makundi madogo ili kupata kundi kubwa
·        Kugawa baadhi ya makundi ikiwa ni makubwa ili yahamishiwe kwenye mizinga iliyohamwa. 
·        chunguza kama nyuki wanajenga masega vizuri kwehye vinzi au miche na siyo kwa kukatiza
·        usafi wa shamba

Msimu wa maua
Wakati huu vichaka vingi na mimea mingi inatoa maua,  nyuki wanakusanya chakula(mbochi na chavua ) kwa wingi pamoja na kuivisha asali.
Shughuli za kufanya katika kipindi hiki ni zifuatazo:
·        kupanua viota (kwa mizinga ya biashara), ina maana kuwa kama sanduku la chini limekaribia kujaa yaani liko robo tatu basi uongeze jingine la ziada juu yake baada ya kuweka kitenga malkia.
·        Kuangalia maadui.
·        Kuangalia kama asali imeshaiva na tayari kwa kuvuna
·        Kutafuta soko la kuuzia mazao yako(Asali,Nta,Gundi n.k)

Makala hii itaendelea tena………….
Imeandaliwa kwa Msaada wa kitabu cha  (R.P.C Temu,2007 ). Na msaada wa Mtandao/Internet.

Kwa Maoni /Ushauri: +255714759047/+255768937884

                        fabianbalele@gmail.com